MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro Bw Nurdin Babu ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kwa kushika nafasi ya kwanza katika Mashindano ya Kitaifa ya Usafi na Mazingira katika kundi la Manispaa nchini.
Aidha ameipongeza Manispaa kwa kutoa Mtaa msafi nchini ambao Mtaa wa Rengua uliopo kata ya Mawenzi.
Babu alitoa pongezi hizo wakati akipokea tuzo hizo kutoka kwa Uongozi wa Manispaa ambapo aliwataka viongozi na watumishi wote wa Manispaa kuendelea kujituma ili kulinda heshima waliyoipata.
“Ushindi huu mlioupata ni mkubwa kwenu na Mkoa wetu kwa jumla; kikubwa hapa ni kudumisha mshikamano, umoja na kuheshimiana miongoni mwenu wakati mkitekeleza majukumu yenu kwani hayo ndiyo yaliyowawezesha kupata heshima hii kubwa”, alisema Babu
Vile vile aliwapongeza wananchi wa Manispaa ya Moshi kwa kushirikina na viongozi wao kwa kufanya usafi kuwa ni moja ya kipaumbele chao jambo ambalo limepekea ushindi huu.
“Usafi unaanzia mtu alipo kwa maana ya kuwa unaanzia majumbani mwetu, hivyo tuilinde heshima hii ya kitaifa tuliyoipata; mbali na ushindi huu, pia tukumbuke ya kuwa usafi unatuhakikishia afya njema ambayo itatuwezesha kutekeleza majukumu yetu”, alisema.
Akiongea katika hafla hiyo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi Zuberi Kidumo alisema kuwa ushindi huo ni heshima kubwa kwa wananchi wa Manispaa ya Moshi na anwapongeza kwa mchango wanaotoa linapokuja swala la usafi wa mazingira.
“Nichukue fursa hii pia kutoa pongezi zangu kwa wale wote ambao wanafanya kazi kubwa kwenye magari ya kuzolea taka ambao hatuko
nao hapa kwenye hafla hii; mchango wao ni mkubwa sana linapokuja swala la kuufanya Manispaa ya Moshi kuwa msafi”, alisema.
Awali Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi Bi Mwajuma Nasombe alisema kuwa mafanikio hayo yametokana na mikakati ambayo Manispaa imeweka ambayo inalenga kuhakikisha Manispaa inakuwa Safi kipindi chote cha mwaka.
Mikakati hiyo ni pamoja na kuongeza magari ya kuzolea taka ili kuhakikisha ufanisi katika huduma za kuzoa taka, utenganishaji taka, ubunifu wa michakato ya kuchakata taka pamoja na kuongeza uelewa kwa wakazi wa Manispaa juu ya umuhimu wa kutunza Mazingira na kufanya usafi”, alisema.
Kulingana na Bi Nasombe, Manispaa ya Moshi imenunua gari jipya la kuzoa taka ambalo alisema litaongeza ufanisi katiak shughuli za kukusanya taka mjini Moshi.
MOSHI MANISPAA KILIMANJARO
Sanduku la barua: P.O BOX 318 MOSHI
Simu: +255-027-2752906
simu ya Mkononi: +255-027-274371/4
Barua Pepe: md@moshimc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Manispaa ya Moshi