Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu ameipongeza Manispaa ya Moshi kwa kukabidhiwa tuzo mbili za pongezi za Taifa “Key Performance Indicators” (KPI) kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kutokana na ufaulu mzuri kwa elimu ya msingi na Sekondari.
Akizungumza leo Julai 15, 2025 wakati wa hafla ya kuipokea tuzo hiyo, Babu amesema Manispaa ya Moshi kupitia mkurugenzi wake imeuheshimisha Mkoa wa Kilimanjaro kwa tuzo hizo na kuutaka uongozi wa Manispaa kuendeleza ufaulu huo kila mwaka.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Mwajuma Nasombe ameeleza kuwa mafanikio hayo yamesababishwa na jitihada zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan za kuboresha sekta ya elimu nchini ikiwemo maslahi ya walimu na miundombinu ya elimu.
Pia, ametaja sababu nyingine za mafanikio kuwa ni pamoja na, nidhamu iliyotukuka miongoni mwa watumishi na ushirikiano uliopo baina ya Manispaa hiyo na uongozi wa Mkoa na Chama cha Mapinduzi.
Aidha, Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi, Rose Sandi amesema katika kipindi cha miaka minne hadi kufikia 2024, Manispaa hiyo imekuwa ya kwanza ki mkoa kwa matokeo ya Darasa la nne ambapo 2024 imekuwa ya kwanza kimkoa na kitaifa huku Darasa la saba Manispaa hiyo ikishika nafasi ya kwanza kimkoa na ya nane kitaifa.
Naye, Kaimu Afisa Elimu Sekondari, Salome Msegeya amesema katika kipindi cha miaka minne hadi kufikia 2024, Manispaa hiyo imekuwa na ufaulu wa Zaidi ya Asilimia 90 ambapo kwa kidato cha pili na kidato cha nne huku mwaka 2024 kidato cha nne kikifaulu kwa asilimia 95.55 na kuifanya manispaa kupata tuzo ya KPI.
MOSHI MANISPAA KILIMANJARO
Sanduku la barua: P.O BOX 318 MOSHI
Simu: +255-027-2752906
simu ya Mkononi: +255-027-274371/4
Barua Pepe: md@moshimc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Manispaa ya Moshi