Halmashauri ya Manispaa ya Moshi leo tarehe 27 Septemba 2025 imesaini mkataba wa ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 13.2 na ujenzi wa mifereji ya maji ya mvua yenye urefu wa kilomita 3.9.
Mkataba huo umesainiwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Bi. Mwajuma Nasombe, kwa niaba ya Halmashauri, na Mkandarasi Hari Singh and Son Limited, kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 22. Fedha hizo zinatolewa na Benki ya Dunia kupitia mradi wa TACTIC.
Hafla hiyo imefanyika katika Uwanja wa Michezo wa Shule ya Msingi Msaranga, ambapo Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu, alikuwa mgeni rasmi.
Akihutubia katika hafla hiyo, Mhe. Babu amemtaka mkandarasi kuhakikisha anatekeleza mradi huo kwa haraka na kwa viwango vya ubora vinavyotakiwa ili kuwanufaisha wananchi wa Moshi.
Barabara zitakazojengwa zinapita katika kata za Ng’ambo, Msaranga, Mjimpya, Miembeni, Njoro, Kaloleni, Pasua, Shirimatunda na Karanga. Aidha, mifereji ya maji ya mvua itajengwa katika kata za Mfumuni, Kilimanjaro, Kiusa na Korongoni.
Akizungumza awali, Bi. Nasombe alisema mradi huo unalenga kuboresha miundombinu ya usafirishaji na kupunguza changamoto za mafuriko katika maeneo ya Manispaa ya Moshi. Aliongeza kuwa utekelezaji wake utasaidia kuinua maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkandarasi Hari Singh and Son LTD ameahidi kukamilisha mradi huo kwa wakati na kwa viwango vinavyokubalika ili kuendana na matarajio ya wananchi na wadau wa maendeleo.
MOSHI MANISPAA KILIMANJARO
Sanduku la barua: P.O BOX 318 MOSHI
Simu: +255-027-2752906
simu ya Mkononi: +255-027-274371/4
Barua Pepe: md@moshimc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Manispaa ya Moshi