1.0 Utangulizi:
Halmashauri ya Manispaa ya Moshi ni miongoni mwa Halmashauri saba za Mkoa wa Kilimanjaro. Mji wa Moshi ulianzishwa 1892, ukahamishiwa mahali ulipo sasa toka Kolila Old Moshi (Moshi Vijijini) mwaka 1911. Mwaka 1926 ulipewa hadhi ya Mji mdogo na mwaka 1956 ukapewa hadhi ya Mji kamili. Ulipewa hadhi ya kuwa Manispaa mwaka 1988.
1.1 Mipaka na eneo la Manispaa:
Manispaa ya Moshi imezungukwa na Wilaya ya Moshi Vijijini kwa upande wa Kusini, Mashariki na Kaskazini, upande wa Magharibi imepakana na Wilaya ya Hai. Mji wa Moshi una eneo la km za mraba 58, na upo kati ya mwinuko wa mita 700 Kusini hadi 950 Kaskazini toka usawa wa bahari. Kila km. moja ya mraba in jumla ya wakazi wapatao 3,165.
1.2 Utawala:
Manispaa ya Moshi imegawanyika katika Tarafa 2, Kata 21 na Mitaa 60 na ina Jimbo moja la uchaguzi. Manispaa ina jumla ya Madiwani 29, kati yao 21 ni wa kuchaguliwa, Viti Maalum wako 7 na Mbunge mmoja wa kuchaguliwa.
1.3 Idadi ya watu:
Manispaa ya Moshi imekua kutoka Mji mdogo uliokuwa na wakazi 8,048 mwaka 1948 na kufikia wakazi 184,292 Kulingana na sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 ambapo inajumuisha wanawake 95,118 na wanaume 89,174.
Tofauti na miji mingine nchini, makisio sahihi ya idadi ya watu yanapaswa kuhusisha watu zaidi ya 76,000 ambao wanatumia muda wa mchana mjini kwa shughuli za biashara na kufaidi rasilimali za Manispaa lakini wanaishi maeneo yanayopakana na Manispaa ya Moshi Vijijni na Hai. Watu hawa hawapo kwenye bajeti hasa kwa mfumo wa LGCDG na programu nyingine zinazotoa ruzuku kulingana na idadi ya watu waliopo.
MOSHI MANISPAA KILIMANJARO
Sanduku la barua: P.O BOX 318 MOSHI
Simu: +255-027-2752906
simu ya Mkononi: +255-027-274371/4
Barua Pepe: md@moshimc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Manispaa ya Moshi