WANAFUNZI 29,000 wa shule za msingi katika Manispaa ya Moshi, wameanza kunufaika na mpango wa taifa wa kudhibiti magonjwa yasiyopewa kipaumbele, baada ya Wizara ya Afya kuendesha zoezi maalumu la ugawaji wa dawa za minyoo ya tumbo na kichocho.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa hiyo, Michael Mwandezi aliyasema hayo jana, wakati akizindua rasmi zoezi hilo litakalozihusisha shule 35 za msingi.
Katika taarifa yake, Mkurugenzi huyo alisema walengwa wa zoezi hilo ni wanafunzi wenye umri kuanzia miaka mitano hadi 14.
"Tutatoa dawa hizo pia kwa watoto wa mitaani wanaoishi katika mazingira hatarishi ambao hawakuandikishwa," alisema Mwandezi.
Ugawaji wa dawa hizo katika shule za msingi umepangwa kufanyika Jumatano ya Aprili 10 na Alhamisi ya Aprili 19, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, magonjwa hayo ni sehemu tu ya magonjwa yale ambayo yalikuwa hayapewi kipaumbele kama vile usubi, trakoma (ugonjwa wa vikope), matende na mabusha.
Hata hivyo, takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha kuwa wanaoathirika zaidi ni wananchi wanaoishi katika mazingira ya umasikini, wanaozungukwa na mazingira machafu na wanaokutana na wadudu wanaosambaza vimelea vya magonjwa hayo.
Taarifa zaidi zinaeleza kwamba magonjwa hayo hayapewi kipaumbele kama magonjwa mengine ya Ukimwi (AIDS) na Kifua Kikuu (TB).
Mwandezi alisisitiza kuwa matatizo ambayo husababishwa na magonjwa ambayo hayapewi kipaumbele ni pamoja na utapia mlo, upungufu wa damu na upofu.
Mengine ni kuathiri ukuaji wa mtoto, gharama kubwa za matibabu, huathiri mahudhurio ya watoto shuleni na husababisha utumbo kuziba kwa minyoo.
MOSHI MANISPAA KILIMANJARO
Sanduku la barua: P.O BOX 318 MOSHI
Simu: +255-027-2752906
simu ya Mkononi: +255-027-274371/4
Barua Pepe: md@moshimc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Manispaa ya Moshi