Halmashauri ya manispaa ya Moshi, imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 334, kwa vikundi 47 vya wanawake,vijana na walemavu, katika manispaa kwa kipindi cha mwaka wa fedha wa 2017/2018.
Hayo yameelezwa na mkuu wa Idara Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii Rose Minja, wakati wa hafla ya kukabidhi hundi kwa ajili ya mikopo hiyo kwa vikundi 20 vya wanawake na vijana kwa robo yanne ya mwaka wa fedha 2017/2018.
Katika hafla hiyo iliyofanyika jana kwenye ukumbi wa Halamshauri, Minja alisema asilimia 72 ya mikopo iliyochukuliwa katika robo ya kwanza hadi ya Tatu ya mwaka huu wa fedha tayari imerudishwa na kwamba pamoja na unafuu wa masharti yake, bado kuna baadhi ya vikundi vinasuasua katika kuteresha mikopo hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kippi Warioba, alitoa wito kwa wanufaika wa mikopo hiyo kujenga tabia ya kuirejesha kwa wakati ili iweze kunufaisha vikundi vingi zaidi kama inavyotarajiwa.
“Nyinyi leo mnanufaika na mikopo hii kwa vile kuna wenzenu waliofanya ustaarabu wakairudisha mikopo waliyokopa kwa wakati, nanyi hamna budi kuirudisha mikopo yenu kwa wakati ili inufaishe wengine wengi zaidi”,alisema.
Awali, mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi,Michael Mwandezi, alisema jumla ya shilingi milioni 100 zimetengwa katika robo ya nne ya mwaka fedha wa 2017/2018 kwa ajili ya mikopo kwa vikundi vya wanawake na vijana manispaa ya Moshi.
“Mikopo hii ni utekelezaji wa sera ya serikali inayozitaka kila Halmashauri nchini kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya mikopo ya wanawake, vijana na walemavu”, alisema na kuongeza wanufaika wote wanatakiwa kuirejesha mikopo hiyo kwa wakati kwa vile si zawadi na kwamba mikopo hiyo iko kisheria kama ilivyo mikopo mingine hivyo masharti yote ni lazima yazingatiwe.
Wakizungumza baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo, walisema, imewasaidia kuanzisha miradi ya maendeleo na kujiajiri wenyewe, hatua ambayo imewawezesha kujikwamua kiuchumi na kuondokana na hali ya utegemezi.
MOSHI MANISPAA KILIMANJARO
Sanduku la barua: P.O BOX 318 MOSHI
Simu: +255-027-2752906
simu ya Mkononi: +255-027-274371/4
Barua Pepe: md@moshimc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Manispaa ya Moshi