WANANCHI wa Kata ya Msaranga, Manispaa ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro wameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zilizofanikisha ujenzi wa shule mpya ya Sekondari ya Msandaka kwenye Kata hiyo.
Pongezi hizo zimetolewa na Diwani wa Kata ya Msaranga Bw Charles Lyimo wakati akizungumzia maendeleo ya shule hiyo baada ya wanafunzi kujiunga na Kidato cha Kwanza kwa mara ya kwanza Januari 9, mwaka huu.
"Shule hii mpya ni ukombozi kwa vijana wa Kata yetu ambao walikuwa wakitembea umbali mrefu Kwenda kwenye Kata zingine kupata elimu ya Sekondari; iliwabidi kuamka saa 10 za usiku na saa 11 za alfajiri ili waweze kuwahi muda uliowekwa wa kufika shuleni", alisema.
Bw Lyimo alisema uanzishwaji wa shule hiyo pia itawawezesha wanafunzi kufanya vyema kwenye masomo yao kutokana na ukweli kwamba watapata fursa ya kujifunza bila ya kuwa na uchovu ambao walikuwa wanapata kwa kuembea umbali mrefu.
"Hata sisi wazazi tumepata nafuu kubwa maana ilikuwa tunatumia gharama kubwa za usafiri ili waweze kuwahi shuleni haswa msimu wa mvua", alisema.
Bw Lyimo pia alipongeza uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kwa kuchangia ujenzi wa Shule hii ya kwanza kabisa katika Kata Msaranga kutokana na fedha za mapato ya ndani za Halmashauri.
"Mchango wa Halmashauri sambamba na ule wa Serikali Kuu umekuja wakati muafaka haswa ikitiliwa maanani ya kuwa Kata yetu haikuwa na shule ya Sekondari kutokana na ile iliyokuweko kupelekwa kata mpya ya Ng'ambo kutokana na mgawanyo uliofanywa na Serikali uliopelekea kuanzishwa kwa kata mpya ya Ng'ambo", alisema.
Akiongelea swala hilo Mkuu wa shule ya sekondari ya Msandaka Bw Erasmus Kyara amesema kuwa ujenzi wa shule hiyo umegharimu jumla ya shilingi milioni 620 kati ya fedha hizo, shilingi milioni 470 zilitolewa na Serikali Kuu na Halmashauri ya Manispaa ya Moshi ilichangia jumla ya shilingi milioni 170 kutoka mapato yake ya ndani
Alisema Awamu ya kwanza ya ujenzi wa shule hii ulihusisha ujenzi wa madarasa nane, meza 160 na viti 160 kwa ajili ya wanafunzi, maktaba, jengo la utawala, jengo la teknolojia ya habari, maabara tatu, vyoo kwa ajili ya wanafunzi na matenki mawili ya maji yenye ujazo wa lita 10,000 kila moja.
Kyara alisema ya kuwa jumla ya wanafunzi 87 walichaguliwa kujiunga na shule hiyo katika kidato cha kwanza kwa mwaka wa 2023 ambapo wanafunzi wasichana walikuwa 51 na wavulana 36. Hadi sasa jumla ya wanafunzi 67 tayari wameanza masomo sawa na asilimia 77 ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na shule hii.
"Uongozi wa Shule kwa ushirikiano na Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Msaranga unaendelea na taratibu za kuwafuatilia wanafunzi ambao walichaguliwa kujiunga na shule lakini bado hawajaripoti; lengo ni kuhakikisha wale wote waliochaguliwa wanajiunga na elimu ya Sekondari", alisema.
Aidha alisema kuwa uongozi wa shule hiyo unaunga mkono wazo la Halmashauri ya Manispaa ya Moshi la kujenga mabweni kwa ajili ya wanafunzi, wazo ambalo alisema litawasaidia wanafunzi kupata muda wa kutosha kujisomea na hivyo kufanya vyema kwenye masomo yao.
Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo akiwemo Nelvin Lyimo, wameelezea kufurahishwa kwao na ujenzi wa shule hiyo katika Kata hiyo, ambapo wamesema kumewapa ari ya kuendelea na masomo yao.
"Shule hii imetusaidia wanafunzi wa Kata ya Msaranga kupata elimu ya Sekondari karibu zaidi ikilinganishwa na wenzetu waliotutangulia madarasa wakati tukiwa shule ya msingi ambao baada ya kuhitimu Darasa la Saba iliwabidi kusoma shule ambazo iliwalazimu Kwenda umbali mrefu sana kwenda na kurudi kutoka shuleni", alisema.
Naye mwanafunzi wa Kidato cha Kwanza Maureen Lyatuu aliipongeza Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zilizopelekea kuanzishwa kwa shule hiyo ambayo alisema pamoja na ukaribu wake ina miundombinu yote muhimu ambayo imefanya mazingira rafiki ya kusomea na uhakika kwa wanafunzi na hii itatusaidia kufanya vizuri kwenye masomo yetu.
Kwa upande wake mwanafunzi mwingine Mwanahawa Bakari alisema ujenzi wa shule hiyo ni jambo la kujivunia kwa Kata hiyo kwani haikuwa na shule ya sekondari ya Serikali na kupelekea wanafunzi waliokuwa wanafaulu katika shule za Msingi za Kata hiyo Kwenda kusoma shule zilizipo kwenye Kata nyingine za mbali na kusababisha usumbufu na gharama kubwa za usafiri kwa wanafunzi.
“Hili ni jambo lakujivunia kwa wanafunzi wanaomaliza Darasa la Saba katika Kata hii ya Masaranga kwani kwa sasa watakuwa na uhakika wa kupata elimu ya sekondari karibu zaidi.”Alisema
MOSHI MANISPAA KILIMANJARO
Sanduku la barua: P.O BOX 318 MOSHI
Simu: +255-027-2752906
simu ya Mkononi: +255-027-274371/4
Barua Pepe: md@moshimc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Manispaa ya Moshi