Manispaa ya Moshi imetekeleza agizo la Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Magufuli la ugawaji wa vitambulisho maalumu kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo ili kuweza kufanya biashara zao kwa uhuru pamoja na kutambulika rasmi.
Zoezi la ugawaji wa vitambulisho limezinduliwa rasmi na Mh. Mkuu wa Wilaya ya Moshi Kippi Warioba kwa kugawa vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo (machinga), ambapo wanafanyabiashara wenye vigezo wapatao 5000 katika Manispaa ya Moshi watanufaika na vitambulishi hivyo.
Akizungumza na wafanyabiashara baada ya uzinduzi wa ugawaji wa vitambulisho hivyo Kippi Warioba, amewataka wafanyabiashara kutumia
vizuri vitambulisho walivyopewa ili kuweza kufikia malengo yao pamoja na malengo ya Serikali ya kuanzisha utaratibuo huo.
Hata hivyo ametoa angalizo kwa wafanyabiashara hao kuendelea kufuata taratibu zilizowekwa na manispaa ikiwemo kuendelea kufanya
biashara zao katika maeneo maalumu yaliyotengwa kwa ajili ya wafanyabisahara wadogo.
Naye Meya wa Manispaa ya Moshi Raymond Mboya aliwapongeza wafanyabishara wadogo kwa jinsi ambavyo wamekuwa wakitekeleza maagizo ya Serikali ikiwemo kufanya biashara zao katika maeneo ambayo wamepangiwa na Serikali.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi Danford Kamenya alisema kuwa Manispaa itahakikisha kuwa vitambulisho vilvyotolewa na Serikali wanapatiwa walengwa ili kutimiza malengo ya Rais wa awamu ya tano ya kuwasaidia wanyonge yanafikiwa na siyo vinginevyo.
“Tumeweka utaratibu mzuri kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) na ofisi zetu za kata na tutahakikisha wafanyabiashara wadogo wenye sifa tu ndiyo wakaopata vitambulisho hivi kwani tumebaini kuwa kuna baadhi ya wafanyabishara wasio na sifa kutaka kufanya ujanja ujanja ili waweze kupata vitambulisho hivi”Alisema..
Kwa upande wa wafanyabaishara wadogo wameishukuru serikali kwa kuwakumbuka na kuwapatia vitambulisho hivyo na kusema kuwa vitambulisho hivi vitawaondolea adha walizikuwa wanakumbana nazo na vile vile vitawasaidia kufanya biashara zao kwa uhuru kwani kwa sasa wanatambuliwa na Serikali.
MOSHI MANISPAA KILIMANJARO
Sanduku la barua: P.O BOX 318 MOSHI
Simu: +255-027-2752906
simu ya Mkononi: +255-027-274371/4
Barua Pepe: md@moshimc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Manispaa ya Moshi