WAKAZI WENGI WA MANISPAA YA MOSHI WAKABILIWA NA CHANGAMOTO YA UZITO MKUBWA
Posted on: September 29th, 2023
UZITO mkubwa ni chanzo cha matatizo mbalimbali yanayowakabili watu wazima pamoja na baadhi ya watoto, katika Manispaa ya Moshi hali ambayo husababisha kasi ya kuongozeka kwa magonjwa yasiyoambukiza kama Shinikizo la damu na Kisukari.
Hayo yamebainishwa na Afisa Lishe wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi,Bi Hadija Kitumpa wakati wa Kikao cha Kamati ya Lishe kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Manispaa ya Moshi.
Alieleza kuwa changamoto ya uzito mkubwa inasababishwa na Ulaji usiofaa na kutokuzingatia Lishe bora, Utumiaji wa pombe kupita kiasi na kutokufanya Mazoezi.
Kitumpa alishauri kuwa watu wote wanatakiwa kuzingatia lishe bora kwa kula mlo kamili wenye makundi matano ya Chakula, kufanya mazoezi, kupunguza unywaji wa pombe kupita kiasi na kuepuka vyakula vilivyosindikwa.
Aidha alitoa wito kwa wakazi wa Manispaa ya Moshi kujenga tabia ya kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kujua afya zao.