Halmashauri ya Manispaa ya Moshi imetoa mikopo ya kiasi cha Tsh. 2,101,740,000 katika kipindi cha mwaka 2015 hadi Machi 2021 ikiwa ni azma ya utekelezaji wa agizo la serikali la kuzitaka kila Halmashauri kutenga asilimia kumi (10%) ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kutuo mikopo ya kuwawezesha Wanawake,Vijana na Walemavu.
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Bi. Rose Minja ameeleza kuwa mikopo hiyo imetolewa kwa vikundi vya wajasiriamali wa Manispaa ya Moshi ambapo Vikundi 292 vya wanawake vimepata Ths 1,549,502,000, Vikundi vya vijana 79 vimepewa Ths 523,322,000 na vikundi vya watu wenye ulemavu 7 vimepata kiasi cha Ths 29,000,000.
Bi Rose Minja ameeleza hayo wakati wa kukabidhi Mikopo ya kiasi cha Tsh 295,290,000 zilizokopeshwa kwa Vikundi 47 vikiwemo 31 vya wanawake na 16 vya vijana kwenye Maadhimisho Siku ya Wanawake Duniani iliyofanyika kwenye Viwanja vya Uhuru Park Manispaa Moshi
Mkuu wa Wilaya ya Moshi Alhaji Rajab Kundya amewaasa wanavikundi waliopewa mikopo hiyo kutumia fedha hizo katika shughuli mbalimbali za kiuchumi walizokusudia kufanya na si vinginevyo.
“Ninawaomba muache kufikiri kuwa fedha hizo mnapewa kama zawadi ambazo mnaweza kuzitumia mnavyopenda, bali mnatakiwa kuzitumia fedha hizo kwa shughuli za kiuchumi zilizokusudiwa na kuzirejesha kwa wakati ili ziweze kukopeshwa kwa vikundi vingine”Alisema Alhaji Rajabu Kundya
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi Juma Raibu Juma ameeleza kuwa Halmshauri itahakikisha itatimiza matakwa ya sheria kwa kuwakopesha asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa mwaka huu wa fedha 2020/2021.
“Hata kama tuna changamoto nyingi tutahakikisha tunaendelea kutoa mikopo hii na tunawaomba msituangushe kwani sisi tunatimiza wajibu wetu na nyie mtimize wajibu wenu wa kutumia fedha hizi vizuri kwa ajili ya maendeleo yenu na kuzirejesha ili zoezi hili la kukopesha vikundi liwe endelevu “Alisema Mstahiki Meya
Bi Emeresiana Shirima anaishukuru Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Mh Rais Dr John Joseph Magufuli kwa kuwajali na kuwapa mikopo isiyo na riba na yenye masharti nafuu ambayo itatuwezesha kutuinua kiuchumi na tunaahidi tutahakikisha kuwa tutarejesha kama ilivyo kwenye mikataba.
MOSHI MANISPAA KILIMANJARO
Sanduku la barua: P.O BOX 318 MOSHI
Simu: +255-027-2752906
simu ya Mkononi: +255-027-274371/4
Barua Pepe: md@moshimc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Manispaa ya Moshi