Halmashauri ya Manispaa ya Moshi imezindua rasmi majukwaa ya kuwawezesha wanawake kiuchumi katika ngazi ya Kata ikiwa ni moja ya malengo yake ya kuwawezesha wanawake kiuchumi.
Katika kutekeleza mpango wake Manispaa ya Moshi imeanzisha na kuzindua majukwaa tisa kwenye kata za Rau,Mfumuni, Karanga,Msaranga,Pasua, Bomambuzi, Majengo, Mimbeni,na njoro ambapo lengo kuu ni kuanzisha majukwaa katika kata zoete 21 za Manispaa hadi kufikia mwezi novemba mwaka huu.
Akizindua majukwaa hayo Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii Manispaa ya Moshi, Rose Minja alisema zaidi wanawake 6000 watanufaika na mpango huo wenye lengo la kuleta mwanga mpya kwa wanawake pamoja na kutumia ujuzi walionao kujikwamua kiuchumi.
Alisema malengo mengine ya kuanzishwa kwa majukwaa ya wanawake ni kuwaunganisha wanawake katika ngazi zote ili waweze kuwa na uelewa juu ya masuala mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa masoko,uibuaji wa fursa,shughuli za ujasiaramali,fursa za mikopo,pamoja na kupeana uzoefu katika uendeshaji wa vikundi kama VICOBA na SACCOS.
Katika hatua nyingine, Rose alisema ili wanawake waweza kujikwamua kiuchumi ni lazima wawe mstari wa mbele kupinga mila potofu na kandamizi ambazo zimepitwa na wakati kwa ajili ya kuleta mabadiliko ya kijamii na kiuchumi.
“Katika kufanikiwa haya yote ni lazima wanawake wajitambue, wawe tayari kukubali mabadiliko,wapendane, waweze kujua mahitaji yaliyopo sokoni, waweze kulipa kodi kwa maendeleo ya taifa pamoja na kufanya ushindani wenye tija”Alisema Rose.
Ili kuweza kufanikisha malengo yake Manispaa ya Moshi inashirikiana na taasisi mbalimbali ikiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau mbalimbali katika utekelezaji wa mpango huo.
Miongoni mwa mashirika yanayoshirikiana na Mansipaa ya Moshi ni shirika la kuhudumia viwanda vidogo SIDO,pamoja na taasisi za kifedha kwa ajili ya kutoa elimu kuhusiana na masuala ya ujasiriamali,utafutaji wa masoko,uanzishwaji wa viwanda vidogo,pamoja na kuwaunganisha wajasiriamali na mamlaka ya chakula na dawa TFDA pamoja na mamlaka ya viwango nchini TBS.
MOSHI MANISPAA KILIMANJARO
Sanduku la barua: P.O BOX 318 MOSHI
Simu: +255-027-2752906
simu ya Mkononi: +255-027-274371/4
Barua Pepe: md@moshimc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Manispaa ya Moshi