WANANCHI wa Kata ya Shirimatunda Manispaa ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro wameipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi Millioni 500 zilizopelekea uboreshaji wa miundombinu ya zahanati ya Shirimatunda, iliyoko kwenye Kata hiyo.
Akitoa pongezi hizo kwa niaba ya wananchi hao, Diwani wa Kata ya Shirimatunda Bw. Francis Shio amesema kuwa maboresho hayo ni faraja kubwa kwa wananchi wa Kata hiyo na zingine za jirani zikiwemo za wilaya za jirani.
“Maboresho ya miundombinu yaliyofanywa na Serikali katika zahanati hii ni sehemu ya huduma za Serikali ambazo zimewanuwaisha na zimewaridhisha wananchi wa Kata yetu na wale wa Kata za jirani”, amesema Mhe Shio.
Amesema kuwa mbali na wakazi wa Kata ya Shirimatunda, pia zahanati hiyo inawahudumia wananchi wa wilaya ya Hai katika vijiji vya Shirimatunda (Hai), Shirimgungani (Hai) na Mijengweni (Hai) na kijiji cha Chekereni katika wilaya ya Moshi.
Mhe. Shio aliendelea kusema kuwa kwa upande wa manispaa ya Moshi, zahanati hiyo inawahudumia wananchi wa Kata za Soweto, Karanga na Shirimatunda yenyewe.
“Nichukue nafasi hii kwa niaba ya wananchi kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha hizi za ujenzi na kwa maono na mawazo yake chanya yanayolenga kuboresha sekta ya afya hapa nchini ikiwemo kuleta wataalam wa afya, kwani yanajibu kero za wananchi kwa vitendo”, amesema Diwani Shio
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi kati zahanati hiyo Dkt. Edna Silayo, amesema maboresho ya miundombinu katika zahanati hiyo yamesaidia kuongeza ari ya watumishi katika zahanati hiyo.
“Jumla ya shilingi Millioni 500 zilizotolewa na Serikali zimewezesha ujenzi Jengo la wagonjwa wanje, Jengo la Maabara, Jengo la kufulia,Jengo la Mama na mtoto na chumba cha upasuaji, pamoja na njia za kutembelea kwa miguu na Kichomea taka cha kisasa hali hii imechangia kuongeza ari ya watumishi kwani hata nafasi za kutolea huduma zimeongezeka”, alisema.
Amesema kabla ya hapo wafanyakazi walikuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu kutokana na ufinyu wa nafasi ambayo ilikuwa inasababishwa na ufinyu wa majengo ya kutolea huduma.
“Tulikuwa hatuna maabara nzuri wala jengo la kuhudumia wagonjwa wa nje, badala yake huduma hizi zilikuwa tunazitolea kwenye chumba kimoja kwa kila idara”, amesema Dkt Silayo
Aliendelea kusema kwa baada ya ujenzi wa jengo la OPD na maabara kukamilika, jengo la zamani la OPD kwa sasa linatumika kwa ajili ya huduma za wazazi (Kliniki ya wajawazito) pamoja na huduma za wale wenye upungufu wa kinga mwilini.
“Maboresho haya hayajawanufaisha wahudumu wa afya tu bali pia wananchi ambapo wale wanaofuatilia huduma tunazotoa hapa idadi yao imeongezeka kutoka wastani wa kati ya watu 20 hadi 25 kwa siku na kufikia wastani wa watu kati ya 25 hadi 40 kwa siku”, Dkt Silayo amesema.
“Kwa sasa wigo wa maeneo ya kutolea huduma umeongezeka kutokana na Serikali kutoa fedha ziliziopelekea ujenzi wa majengo haya ya ziada na ndiyo maana watu wanaamua kufuata huduma hapa ambapo ni karibu na maeneo wanayoishi”, a.
Mmoja wa wananchi wa eneo hilo Bi Liana Ndanshau ameipongeza Serikali kwa maboresho hayo ambayo amesema yamewasaidia kupata huduma muhimu na kwa haraka haswa nyakati za jioni au usiku.
“Tulikuwa tunapata wakati mgumu pale mtu unapokuwa na dharura ya ugonjwa au hata mwenzako au jirani ambaye ni mgonjwa, ilikuwa inatulazimu kutafuta njia za haraka kufuata huduma nje ya hapa lakini kwa maboresho haya, hayo yatakuwa ni historia”, Amesema Bi Liana
MOSHI MANISPAA KILIMANJARO
Sanduku la barua: P.O BOX 318 MOSHI
Simu: +255-027-2752906
simu ya Mkononi: +255-027-274371/4
Barua Pepe: md@moshimc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Manispaa ya Moshi