Halmashauri ya Manispaa ya Moshi imefanikiwa kupata kiasi cha Tsh Milioni 42 kama mapato ya ndani baadaya ya kuzalisha na kuuza tani 157 za mbolea ya mboji kwenye kiwanda chake kilichopo eneo la Mtakuja katika kipindi cha Desemba 2020 na Aprili 2022.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Idara ya usafi na mazingira Bi Viane Kombe wakati akiwasilisha taarifa ya mradi huo katika ukumbi wa Manispaa kwa Mstahiki Meya wa Jiji la Tubingen nchini Ujerumani Bw Boris Palmer, na madiwani kutoka Tubingen walipotembelea hamashauri ya Manispaa ya Moshi.
“Mradi huu mbali na kuiingizia halmashauri mapato, pia umechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha mazingira wilaya ya Manispaa ya Moshi kwa ujumla kutokana kuwa unatumia malighafi ambazo ni taka zinazozalishwa kufuatia matumizi ya matunda na mbogamboga”, alisema Bi Viane
“Jumla ya tani 236 za taka ngumu huzalishwa Manispaa ya kila siku ambapo katika kipindi hicho cha mwaka mmoja jumla ya tani 2,058 za mbogamboga na matunda zilitumika kuzalisha mbolea ya mboji kupitia mradi huu”, alisema.
Bi Kombe aliendelea kueleza kuwa katika kufannya mradi huo kuwa endelevu, baadhi ya mikakati imekuwa ikitekelezwa ikiwemo kutoa elimu kwa wanafunzi wa shule za msingi ili kujenga kizazi kijacho kitakachokuwa na uelewa mpana wa utunzaji wa mazingira.
“Wanafunzi katika Vilabu 45 mazingira kutoka shule 20 za msingi wamepatiwa mafunzo kuhusu kutengeneza mbolea ya mboji na kutenganisha taka ngumu ambazo ni malighafi ya kutengenezea mbolea ya mboji”, alisema.
Kupitia mradi huu wanafunzi wamepata elimu pamoja na kushirikishwa katika zoezi la kupanda miti na kuitunza kwa kutumia mbolea ya mboji katika maeneo ya shule.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo Meya wa Jiji la Tubingen Mhe. Boris Palmer alielezea kuridhishwa kwake na utekelezaji wa mradi huo ambao unaendeshwa kupitia ufadhili wa Jiji hilo kwa kushirikiana na Manispaa ya Moshi kutokana na undugu ulioko kati ya Jiji la Tibingen na Manispaa ya Moshi.
“Ni furaha kwangu mimi kuona ya kuwa mradi huu umelepata mafanikio makubwa, haswa ikitiliwa maanani nilikuja hapa mwaka wa 2010 kwa ajili ya kuanza mikakati ya kuuanzisha”, alisema Palmer
Aliongeza, “Mradi huu ni kielelezo tosha ya jinsi watu kutoka nchi mbili tofauti tena kutoka mabara mawili tofauti wanavyoweza kushirikiana kupitia halmashauri zao kwa ajili ya kuleta maendeleo kwa watu wote tena kwa mafanikio makubwa”.
“Mbali na mradi huu pia tumejenga mahusiano mazuri kati yetu ambapo kwa sasa kahawa inayotoka mkoani Kilimanjaro inauzwa katika Jiji la Tubingen na hivyo kuwaingizia mapato wakulima wa kahawa na mapato na Taifa”, alisema.
Kwa upande wake Kaimu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Mhe Stuart Nkinda alipongeza uongozi na wananchi wa Jiji la Tubingen kwa ushirikiano walioutoa katika kufanikisha mradi huu ambao alisema mbali na kuboresha mazingira na kuingiza mapato pia umechangia kupatikana kwa ajira kwa wakazi wa Manispaa ya Moshi.
MOSHI MANISPAA KILIMANJARO
Sanduku la barua: P.O BOX 318 MOSHI
Simu: +255-027-2752906
simu ya Mkononi: +255-027-274371/4
Barua Pepe: md@moshimc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Manispaa ya Moshi