Mkuu wa Wilaya ya Moshi Kippi Warioba, amewataka wanufaika wa Mfuko wa maendeleo ya Jamii (Tasaf) mpango wa kunusuru kaya maskini, Manispaa ya Moshi,Mkoani Kilimanjaro kutumia fedha wanazozipata, kuanzisha miradi midogomidogo ambayo itawawezesha kujikwamua kiuchumi.
Warioba alisema hayo wakati alipotembelea baadhi ya wanufaika hao,pamoja na kutoa elimu ya awali kabla ya kupewa fedha na kushuhudia walengwa hao walivyonufaika na fedha ambazo wamekuwa wakipewa kwa kuanzisha miradi.
Alisema wapo wanufaika wa Tasaf ambao wametumia fedha walizozipata kuanzisha miradi na kuweza kupiga hatua ya kimaendeleo, hivyo ni vyema wanufaika wote wakaiga mfano huo ili kuweza kuondoka kwenye kundi la kusaidiwa na kuachia wengine kufikiwa.
“Mchango mdogo wa Tasaf mnaoupata utumieni vizuri, msikate tamaa na kubweteka,anzisheni miradi midogo midogo ya maendeleo, ili kuweza
kujiinua kiuchumi, kwani tunategemea baada ya muda msimame wenyewe na
kuendesha maisha yenu bila kutegemea msaada wowote”alisema Warioba.
Akizungumza Mratibu wa mpango wa kunusuru Kaya Maskini Manispaa ya Moshi, Dennis Robert,alisema jumla ya fedha ambazo zimewafikia walengwa 1,461wa mpango huo mpaka sasa ni Sh 1.5 Bilioni katika mizunguko 22.
Alisema mpaka sasa walengwa zaidi ya 200 wameanzisha miradi ya ufugaji wa kuku,bata ,mbuzi na kuanzisha biashara ndogondogo,huku wengine 300 wakijiingiza kwenye kilimo,hatua ambayo imewawezesha kubadilisha maisha yao na kuondoka kwenye mlo mmoja waliokuwa wakiupata na sasa kupata milo mitatu kwa siku.
“Wapo baadhi ya Walengwa wa mpango wa kuzinusuru kaya Maskini,ambao wamepiga hatua kupitia fedha kidogo wanazozipata, wameanzisha miradi na kwa sasa wanapata chakula bila shida, wanasomesha watoto wao na wamewakatia bima za afya, lakini pia ipo changamoto ya uwepo wa watu maskini ambao bado hawajafikiwa”alisema.
Baadhi ya walengwa walisema kupitia fedha kidogo wanazozipata kutoka Tasaf, wameweza kuanzisha miradi ya ufugaji na biashara ndogondogo na kwa sasa wameweza kupiga hatua ya kimaendeleo na hata kununua kiwanja na wengine kuanza ujenzi.
MOSHI MANISPAA KILIMANJARO
Sanduku la barua: P.O BOX 318 MOSHI
Simu: +255-027-2752906
simu ya Mkononi: +255-027-274371/4
Barua Pepe: md@moshimc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Manispaa ya Moshi