Mkuu wa Wilaya ya Moshi Mhe. Abbas Kayanda ameupongeza Uongozi na Menejimenti ya Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kwa kutimiza takwa la kisheria inazozitaka Halmashauri kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuvikopesha Vikundi vya Wanawake, Vijana na watu Wenye Ulemavu.
Kayanda ametoa pongezi hizo wakati akikabidhi mfano wa hundi ya mikopo isiyo na riba kiasi cha Shs. 367,550,000 ambazo zinakopeshwa kwa vikundi 61. Vikundi 42 vya Wanawake vimekopeshwa sh.240,500,000, vikundi 15 vya Vijana vimekopeshwa kiasi cha Shs.119,050,000 na vikundi 4 vya Watu wenye Ulemavu vimekopeshwa kiasi cha Shs 8,000,000.
“Leo ninyi mnanufaika na mikopo hii kwa vile kuna wenzenu waliokopeshwa kipindi kilichopita na wakazitumia kwa malengo yaliyokusudiwa kisha wakairudisha mikopo yao kwa wakati, nanyi hamna budi kuirudisha mikopo yenu kwa wakati ili iweze kuja kuwanufaisha wengine wengi zaidi”,alisema.
Amewataka wote waliopokea mikopo kuhakikisha inawanufaisha katika shughuli za kiuchumi ili waweze kujikwamua kiuchumi na kukua kutoka hatua moja Kwenda nyingine.
“Tunategemea kama kikundi kilikopa kiasi kidogo kifanye shughuli zake vizuri na kurejesha ili kipindi kijacho kiweze kukopeshwa fedha zaidi na kukuza biashara hata kuweza kufungua kiwanda”
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi Mhandisi Zuberi Kidumo alisema kuwa Mikopo hii ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020/2025 na Sera ya serikali inayozitaka kila Halmashauri nchini kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya mikopo ya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu.
“ Tunawaomba wanufaika wote mtambue kuwa mikopo hii ipo kisheria na sio zawadi hivyo mnatakiwa kuitumia vizuri kwa malengo yaliyokusudiwa ili muweze kurejesha kama sheria inavyotaka” Alisema
Awali Kaimu Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii Bw. Denis Shette alisema Katika mwaka wa fedha 2021/2022 robo ya kwanza hadi ya tatu Halmashauri ilifanikiwa kukopesha vikundi 159 kiasi cha sh.949,398,700 ambapo vikundi 116 vilikuwa vya wanawake,32 vya vijana na 11 vya watu wenye ulemavu.
MOSHI MANISPAA KILIMANJARO
Sanduku la barua: P.O BOX 318 MOSHI
Simu: +255-027-2752906
simu ya Mkononi: +255-027-274371/4
Barua Pepe: md@moshimc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Manispaa ya Moshi