MKUU wa wilaya ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro, Mhe. Abbas Kayanda, amewapongeza walimu na uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kwa kazi nzuri na juhudi kubwa walizozifanya katika sekta ya elimu zilizopelekea Manispaa ya Moshi kufanya vizuri kwenye matokeo ya Mtihani wa Kitaifa wa kumaliza Elimu ya msingi
Kayanda alitoa pongezi hizo baada ya kupokea taarifa ya elimu kwa mwaka wa 2022 iliyotolewa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi Rashid Gembe, katika kikao cha Maafisa Elimu, Waratibu Elimu Kata na Watendaji wa kata kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Ofisi ya Mkoa wa Kilimanjaro.
“Ufaulu katika mitihani ya Shule za Msingi kwa Manispaa ya Moshi katika miaka ya hivi karibuni umeipa wilaya ya Moshi heshima ya kipekee katika Mkoa wa Kilimanjaro, ombi langu kwenu msibweteke na mafanikio haya badala yake mzidishe juhudi ili mafanikio haya yafikie ngazi ya Taifa”, alisema.
Mhe.Kayanda alisema kuwa Manispaa ya Moshi imekuwa ikifanya vizuri kwenye mitihani ya kitaifa ya Darasa la Saba katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, huku asilimia ya ufaulu ikiongezeka kitaifa na kimkoa kila mwaka.
“Taarifa za kitaifa zinazohusiana na matokeo ya mitihani ya Darasa la Saba yanaonyesha kuwa Manispaa ya Moshi imeshika nafasi ya tano kitaifa mwaka wa 2020, nafasi ya tatu mwaka wa 2021 na nafasi ya pili mwaka 2022, haya ni mafanikio makubwa ya kujivunia”, alisema.
Akitoa taarifa kwa Mkuu wa Wilaya Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi Bw Rashid Gembe alisema mafanikio hayo yametokana na juhudi mbalimbali zilizofanywa na Manispaa pamoja na walimu .
“Wanafunzi hupata chakula cha mchana kutokana na mpango wa wazazi kuchangia chakula baada ya kupata kibali maalum cha kuchangia chakula kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya”, alisema na kuongeza kwa uchangiaji chakula cha mchana shuleni umechochea kuongeza kiwango cha taaluma miongoni wa wanafunzi wa Shule za Msingi.
Alisema sababu nyingine ni ile ya uboreshaji wa miundombinu ya shule ambapo katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 Manispaa ya Moshi kupitia mapato ya ndani ilitoa jumla ya shilingi milioni 400 zilizotumika kuboresha miundombinu katika Shule za Msingi.
“Katika maboresho hayo, vyoo 60 vimejengwa sambamba na madarasa 11 mapya na mengine mawili yalifanyiwa ukarabati mkubwa; marekebisho haya pia yamechangia kuboresha miundombainu inayotosheleza kupokea wanafunzi wa Darasa la Awali na Darasa la Kwanza mwaka 2023”, alisema.
Aidha alisema hadi kufikia Juni 30, 2022, kwa mwaka wa fedha 2022/2023, jumla ya shilingi 417,359,646.08 zilipokelewa shuleni ikiwa ni Ruzuku ya Elimu Msingi Bila Ada (EMBA) kwa ajili ya maendeleo ya elimu shule za msingi, ambapo alisema kiasi hicho ni sawa na asilimia 97.3 ya kiasi cha 428,874,000 ya fedha zote za EMBA, ambazo ziko kwenye bajeti ya mwaka wa fedha wa 2022/2023
MOSHI MANISPAA KILIMANJARO
Sanduku la barua: P.O BOX 318 MOSHI
Simu: +255-027-2752906
simu ya Mkononi: +255-027-274371/4
Barua Pepe: md@moshimc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Manispaa ya Moshi