Mkuu wa Wilaya ya Moshi Kisare Makori, ameuagiza Uongozi wa Halmshauri Manispaa ya Moshi kuhakikisha unatenga bajeti ya kutosha kulingana na maelekezo ili kusaidia juhudi katika kuboresha huduma za lishe kwa wananchi na kufanikisha mapambano dhidi ya utapiamlo.
Kisare ametoa Rai hiyo leo wakati akifungua kikao cha maandalizi ya mpango na Bajeti ya Lishe kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ambapo amesema Manispaa ya Moshi inatakiwa kuhakikisha Bajeti itayotengwa mwaka huu inakidhi vigezo na inazingatia maoni yalitolewa na wadau katika vikao vya tathmini ya lishe ya Manispaa ya Moshi.
“Tunatambua kuwa lishe duni huathiri ukuaji na maendeleo ya mtoto kimwili na kiakili, hivyo kufifisha mchango wake katika maendeleo ya jamii na Taifa hivyo ni wajibu wetu kutenga bajeti ya kutosha kwa shughuli za Lishe ili tuweze kukabiliana na tatizo la lishe duni na Utapiamlo “Alisema Kisare
Aliendelea kueleza kuwa pamoja na maendeleo ambayo nchi hii imekuwa ikiyapata katika maeneo mbalimbali, bado utapiamlo umeendelea kuathiri jamii, hivyo uboreshaji wa hali ya lishe Nchini ni msingi wa afya njema, ubunifu, maendeleo mazuri ya kiuchumi na kupunguza umaskini kwa mtu mmoja mmoja na Nchi kwa ujumla.
"Matatizo mbalimbali ya utapiamlo yanaendelea kudumaza, kulemaza na hata kuua watoto na wanawake hasa wajawazito na wanaonyonyesha, naomba tuongoze juhudi katika kuboresha shughuli za lishe kwa jamii ya wananchi wa Manispaa ya Moshi,kwani jamii inategemea sana uongozi wetu katika kusimamia vyema mapambano dhidi ya utapiamlo”Alisema
Aidha, Alisema kuwa naamini tukitenga bajeti yenye kutosheleza kwa shughuli za lishe na kuwajibika ipasavyo itasaidia kuimarisha hali ya lishe na kupunguza tatizo la utapiamlo na kusababisha kufikiwa kwa malengo ya maendeleo katika nchi yetu,
Vile Vile ameutaka uongozi wa Manispaa kuhakikisha kuwa fedha za lishe zinatengwa na kutolewa kwa wakati kulingana na bajeti ili kuwezesha shughuli zinazohusiana na lishe kutekelezwa kwa wakati na kufikia malengo yaliyokusudiwa.
MOSHI MANISPAA KILIMANJARO
Sanduku la barua: P.O BOX 318 MOSHI
Simu: +255-027-2752906
simu ya Mkononi: +255-027-274371/4
Barua Pepe: md@moshimc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Manispaa ya Moshi