MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro Bw Nurdin Babu, amewataka wale wote waliopewa majukumu ya kuendesha zoezi la Sensa ya watu na Makazi kutekeleza wajibu wao ipasavyo ili kukamilisha kazi nzuri aliyoifanya Rais Samia Hassan ya kuhamasisha wananchi kushiriki zoezi hilo.
Bw Babu alitoa wito huo wakati alipopokea taarifa ya matayarisho ya zoezi hilo kwa manispaa ya Moshi kwenye kikao cha pamoja kilichofanyika katika ukumbi wa CCM Mkoa.
"Sensa ya watu na makazi ni muhimu kwa Taifa kwa ajili ya Serikali kupanga mipango ya maendeleo; ni kutokana na umuhimu huo Rais Samia alitumia muda mwingi kuhamasisha kuhusiana na zoezi hili kupitia hotuba zake mbalimbali; tukifanikisha zoezi hili tutakuwa tumekamilisha kazi nzuri aliyoifanya", alisema.
Aidha aliwataka wananchi kutokuwa na hofu na maswali yatakayoulizwa kutokana na madodoso yaliyotayarishwa kwa ajili ya zoezi hili na kwamba wanachotakiwa ni kujibu yale ambayo yanawahusu tu.
"Utaulizwa kwa mfano una gari au nyumba na kadhalika; sasa usipate hofu kwamba maswali hayo ni ya nini, iwe unavyo hivyo vitu au la unachotakiwa ni kujibu ndiyo au la, unatakiwa kujibu yale yanayokuhusu tu, majibu utakayotoa hayatakuathiri kwa njia yoyote ile", alisema.
Aidha alitoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano wao wa dhati kwa wale waliopewa dhamana ya kuendesha zoezi hili ili kulifanya iwe rahisi kwao na kwamba kufanikiwa kwake ni mwanzo wa Serikali kupanga mipango bora ya maendeleo ambayo itawahusu wananchi wenyewe.
Pia katika mkutano huo ambao uliwashirikisha viongozi wa mitaa, kata za manispaa ya Moshi alitoa wito kwa wananchi kutokuwaficha wenzao wenye kuishi na ulemavu wa aina yoyote kutokana na ukweli ya kuwa mipango ya maendeleo inawahusu na wao vilevile.
"Nyinyi mnawajua wale wote walioko maeneo yenu ya kiutawala, pale mtakapogundua kuna mtu anaeishi na ulemavu halafu jamaa zake wamemficha ili asihusishwe kwenye zoezi hili muhimu toeni taarifa haraka iwezekanavyo ", alisema.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa amewataka viongozi hao wa Mitaa na wale wa Kata kujenga tabia ya kumsemea Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na kazi nzuri anayoifanya kwa ajili ya Watanzania na Taifa lote kwa ujumla.
"Sisi kama viongozi tunajua kazi nzuri anazofanya Rais lakini si wote walio nje ya uongozi wanaojua hayo, hivyo ni wajibu wenu kila mnapokutana na wananchi huko kwenye maeneo yenu ya kazi mtangaze kazi nzuri zinazofanywa na Rais ili wawe na uelewa na kuepukana na maneno yanayoenezwa na wale wasio na nia njema kwa Serikali wanaosema hakuna kazi zinazofanyika", alisema
Awali akitoa taarifa ya maendeleo ya maandalizi ya zoezi la sensa ya watu na makazi, mratibu wa sensa ya watu na makazi manispaa ya Moshi Bi Lucia Raphael alisema hadi kufikia Agosti 20, 2022, mipango yote ilikuwa imekamilika kwa asilimia kubwa.
"Utengaji wa maeneo madogomadogo ya kijiografia 353 umefanyika na kukamilika katika mitaa yote 60 ndani ya kata zote 21 ndani ya Moshi Manispaa", alisema.
Aidha alisema makarani, wasimamizi maudhui 95, wasimamizi wa TEHAMA 21, makarani wa kawaida 798, makarani wakuu 60 na wakufunzi 54 wameshapatiwa mafunzo kupitia ngazi mbalimbali zikiwa za Wilaya na Mkoa.
"Mafunzo ya vitendo kwa makarani, wasimamizi wa maudhui na TEHAMA yalifanyika kwa siku 19 na mazoezi ya vitendo kufanyika katika Kata za Rau, Korongoni, Soweto, Karanga, Longuo B na Bomambuzi", alisema.
MOSHI MANISPAA KILIMANJARO
Sanduku la barua: P.O BOX 318 MOSHI
Simu: +255-027-2752906
simu ya Mkononi: +255-027-274371/4
Barua Pepe: md@moshimc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Manispaa ya Moshi