Mkuu wa Kilimanjaro, Nurdin Babu ametangaza kuwa kila siku ya Jumamosi itakuwa siku maalumu ya kufanya usafi kwa wakazi wa Manispaa ya Moshi.
Babu ametoa agizo hilo leo Jumamosi tarehe 8/10/22 kwenye uzinduzi wa zoezi la kufanya usafi lililofanyika katika soko na Mbuyuni na Manyema kata ya Bondeni Manispaa ya Moshi kwa lengo la kuwakumbusha wananchi wa Manispaa ya Moshi kuendelea na utamaduni wa kudumisha usafi na kutunza Mazingira.
“Natambua kuwa huwa mnafanya usafi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi na leo hii nimezindua rasmi zoezi la kufanya usafi kila Jumamosi , hili ni agizo kwani tunataka kuendeleza heshima ya Manispaa ya Moshi ya kuongoza kwa usafi nchini kila mwaka.Ni wajibu wa kila wananchi kushiriki zoezi hili kikamilifu na kuhakikisha kuwa sehemu anayokaa au kufanya shughuli zake za kiuchumi au kijamii inakuwa safi” Alisema
Aidha amewataka wananchi wote kuhakikisha kuwa kila Jumamosi hakuna kufungua biashara au ofisi kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa 3 kamili kwani muda huu utakuwa ni muda wa kufanya usafi tu.
Mkuu wa Mkoa ameeleza kuwa Serikali haitaki kugombana na watu hivyo anawaomba wananchi kuzingatia maagizo hayo kwani atakuwa anapita kila siku ya jumamosi akiwa na jeshi la akiba ili kukagua na kuangalia utekelezaji wa agizo lake.
Babu amesema katika siku hiyo, kila mmoja anapaswa kutekeleza wajibu wake kuanzia ngazi ya kaya, Mtaa na Kata na kuwataka wananchi kujumuika katika kufanya usafi.
Uzinduzi wa Zoezi hilo la usafi lililoongozwa na Mkuu wa Mkoa liliwahusisha Mkuu Wilaya ya Moshi ,Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi , Mkurugenzi wa Manispaa ,Waheshimiwa Madiwani, Jeshi la Zimamoto na Jeshi la Akiba, Uhamiaji, Jeshi la Polisi, Watendaji wa Halmashauri na Mamlaka ya Maji Safi na Utunzaji wa Mazingira, Wafanyakazi kutoka Bonde la Mto Pangani, Benki ya NMB, Benki ya Mkombozi na wananchi.
MOSHI MANISPAA KILIMANJARO
Sanduku la barua: P.O BOX 318 MOSHI
Simu: +255-027-2752906
simu ya Mkononi: +255-027-274371/4
Barua Pepe: md@moshimc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Manispaa ya Moshi