Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kwa kufanikiwa kukusanya mapato ya ndani hadi kufikia asilimia 101 na kuitaka kuongeza ubunifu na kubuni vyanzo vipya vya mapato, ili kupanua wigo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani, kutoka Sh billioni 8.9 zilizokusanywa mwaka wa fedha 2023/2024 hadi kufikia Sh bilioni 10 mwaka huu wa fedha 2024/2025.
Akizungumza kwenye kikao maalumu cha baraza la Madiwani cha kujadili hoja na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa , Babu ametaka kuwepo kwa ubunifu wa vyanzo vipya vya mapato vitakavyozingatia pia falsafa ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kujenga urafiki na mazingirira mazuri baina ya wafanyabiashara na wakusanyaji wa maduhuli ya Serikali.
"Nilikuwa ninashida sana pale ofisini, nilipoletewa taarifa Manispaa ina asilimia 32 ya ukusanyaji wa mapato hadi Desemba 2023, ambayo ilikuwa ni nusu mwaka, nikasema hii ni hatari kubwa, lakini niwapongeze kwa jitihada kubwa mlizozifanya hadi kuweza kufikia malengo na hata kuyavuka kwa kukusanya kwa asilimia 101"amesema Babu na kuongeza kuwa,
"Kama mmeweza kukusanya asilimia 70 kwa miezi sita ni dhahiri kabisa mnaweza kukusanya zaidi, sasa niombe mbuni vyanzo vipya vya mapato, lakini pia katika hili, mjenge ushirikiano na kuwa karibu na wafanyabuashara ili tuweze kutoka kwenye Sh billioni 8 na kufukia Sh billioni10, mkikusanya vizuri, mtapanga jambo mnalolitaka nyie na kuongeza kasi ya maendeleo".
Katika hatua nyingine, Babu ameutaka uongozi wa Manispaa hiyo, kuhakikisha kuwa wapangaji wa majengo na vibanda vya biashara vya Halmashauri wanalipa kodi zao kwa wakati.
"Kuna hoja hapa tunawadai watu, hivi mtu umempangia kwenye nyumba yako halafu hataki kukulipa, mimi nataka kuwashauri na ni ushauri wa bure, Mkurugenzi simama kidete, mtu ambaye hataki kulipa kwenye majengo ya Halmashauri, wewe agana nae mapema na kwangu wakija wataishia getini".
Awali akitoa taarifa ya ukusanyaji wa mapato, Mkurugenzi wa Manispaa Mwajuma Nasombe, amesema hadi kufikia Juni 30 mwaka 2024 Manispaa imefanikiwa kukusanya mapato ya ndani zaidi ya Sh bilioni 8.9 ambayo ni sawa na asilimia 101 ya malengo yaliyokuwa yamekusudiwa.
"Lengo letu ilikuwa ni kukusanya Sh billion 8.8 na mpaka Juni 30, 2024 tumefanikiwa kukusanya Sh billioni 8.9 sawa na asilimia 101, ni mafanikio makubwa kwetu, tuendelee kushirikiana kama watendaji na madiwani, katika kuhakikisha tunaendelea kuongeza ukusanyaji wa mapato"
Naye Meya wa Manispaa Moshi Mhandisi Zuberi Kidumo, ametaja umoja na ushirikiano baina ya Madiwani na watendaji wa Halmashauri na elimu kwa umma kuwa ni miongoni mwa siri ya mafanikio ya kuongeza ukusanyaji wa mapato.
"Nimpongeze mkurugenzi na menejimenti yake kwa makusanyo, hii ni hustoria, tunaamini tukijipanga na tuna uwezo wa kuvunja tena rekodi hii kwa mwaka huu mpya wa fedha, na haya ndiyo mambo yatakayosaidia kuweza kutekeleza miradi ambayo tumeipanga ".
Mbunge wa Moshi Mjini Priscus Tarimo, amesema endapo madiwani na watendaji wataendelea kuwa na mshikamano wa pamoja Manispaa hiyo ina uwezo wa kuongeza ukusanyaji wa mapato zaidi na hatimaye kufikia ndoto ya Manispaa ya Moshi ya kuwa Jiji kwa haraka zaidi.
"Mwezi Desemba Manispaa ya Moshi tulikuwa wa Mwisho hapa mkoani kwa makusanyo kwa asilimia 32 lakini kwa kipindi kifupi cha miezi sita, tumeweza kufanya vizuri sana, hii inatupa tafsiri kwamba tuna uwezo wa kwenda mbali zaidi ya hapa tulipo na tukiweza kusogeza hili la mapato hata ndoto yetu ya jiji itakuja haraka zaidi".
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Zephania Sumaye, ameupongeza uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kwa mafanikio hayo huku akiwataka kuongeza juhudi zaidi.
"Niwapongeze Manispaa kwa kuweza kuongeza ukusanyaji wa mapato na kwa kasi mliyo nayo kwa sasa mnaweza kuongeza zaidi na mkakusanya zaidi ya hii, mimi siyo nabii wala sina vinasaba vya unabii, lakini kwa kasi ya mkurugenzi huyu, ninaamini kwa mwaka huu wa fedha tutakusanya kama mlivyokusanya hii asilimia 70 kwa nusu ya kwanza na nusu ya pili asilimia 70 hivyo kukusanya kwa asilimia 140 ya malengo tuliyojiwekea" Alisema Sumaye
MOSHI MANISPAA KILIMANJARO
Sanduku la barua: P.O BOX 318 MOSHI
Simu: +255-027-2752906
simu ya Mkononi: +255-027-274371/4
Barua Pepe: md@moshimc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Manispaa ya Moshi