Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mh. Seleman Jafo amefanya ziara katika kituo kikuu cha mabasi kilichopo Manispaa ya Moshi na kusisitiza kuanza haraka kwa wakati ujenzi wa kituo kipya cha mabasi cha Ngangamfumuni kitakachogarimu tsh bilioni 27.
Akiwa katika kituo kikuu cha Mabasi Waziri Jafo alisema Manispaa imefikia katika hatua nzuri kwa kumpata mkandarasi wa ujenzi,ambapo tayari Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni saba kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha kisasa cha mabasi.
Waziri Jafo pia aliitaka Manispaa ya Moshi kuharakisha mchakato wa kuanza kwa ujenzi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha malengo ya fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa mradi huu yanafikiwa na endapo Manispaa itaendelea kuchelewa kutumia fedha hizo Serikali haitasita kuzihamishia fedha hizo kwenye Halmashauri nyingine.
Kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Moshi, Raymond Mboya, alisema miongoni mwa mambo yanayoweza kusababisha kuchelewa kuanza kwa ujenzi wa kituo cha Ngangamfumuni ni pamoja na kusubiriwa kwa kibali kutoka hazina.
“Tayari Serikali imekwishatoa kiasi cha tsh bilioni 7 lakini tunajua kuwa ujenzi wa kituo hiki utagharimu zaidi ya bilioni saba tunakuomba utusaidie kusukuma ili tuweze kupata kibali toka hazina kitachotuwezesheza kukopa fedha kutoka benki ya TIB ili ujenzi wa kituo uweze kukamilika kwa wakati”Alisema Mboya.
Akitoa taarifa ya Mradi wa Ujenzi wa kituo kipya cha mabasi cha Ngangamfumuni Mkurugenzi wa Manispaa Michael Mwandezi alisema kuwa tayari tumekwishampata mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha hicho na tunatarajia ujenzi utaanza rasmi mwenzi Januari mwaka 2019.
“Mh Waziri tunakuhakikishia kila kitu kinaenda vizuri na mchakato wa kumpata mkandarasi ulizingatia taratibu zote za manunuzi ikiwa ni pamoja na kushirikisha viongozi ngazi ya Mkoa ambapo mwezi Januari tutasaini mkataba na mkandarasi kwa ajili ya kuanza ujenzi”Alisema Mwandezi.
Baadhi ya wadau wa usafirishaji wameeleza kuwa kujengwa kwa kituo kipya cha mabasi kutapunguza kero ya msongamano iliyopo katika kituo kikuu cha mabasi kinachotumika kwa sasa hivyo kuomba Serikali kuharakisha ujenzi wake.
MOSHI MANISPAA KILIMANJARO
Sanduku la barua: P.O BOX 318 MOSHI
Simu: +255-027-2752906
simu ya Mkononi: +255-027-274371/4
Barua Pepe: md@moshimc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Manispaa ya Moshi