Mbunge Moshi Mjini Mhe. Priscus Tarimo amempongeza Mkurugenzi na Menejimenti ya Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa Manispaa.
Amesema kwa kipindi cha Miaka 3 ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan serikali imetoa fedha za miradi ya Maendeleeo zaidi Sh. Billioni 23 ambazo zimetumika katika ujenzi wa Shule Mpya, Madarasa, Jengo la Utawala, Vituo vya afya na hospitali ya Manispaa.
Tarimo ameyasema hayo leo, Julai 11, 2024 wakati wa uzinduzi wa Madarasa 9 shule ya Sekondari Mawenzi ambao utekelezaji wake umegharimu zaidi ya Sh,234 milioni.
Mbunge Tarimo alitembelea na kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa ndani ya Manispaa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa hospitali ya Manispaa, bweni la wavulana shule ya Sekondari Msandaka, shule ya Sekondari Lucy Lameck, Ukarabati wa shule ya msingi Mwenge, ujenzi wa jengo la utawala la Manispaa hiyo ambalo limegharimu zaidi ya Sh2 bilioni.
"Leo tulikuwa tunakagua miradi ambayo inatekelezwa na serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, miradi hii imejengwa kwa ubora na kwa kiwango kinachotakiwa,"
Amelipongeza baraza la Madiwani, Mkurugenzi na Menejimenti ya Manispaa kwa kusimamia vizuri na kwa ubora ujenzi wa miradi hiyo na kwamba ameridishwa nayo kutokana na kasi ya ujenzi huyo ambao amesema serikali imeleta fedha kwa ajili ya kuhakikisha kipaumbele cha elimu pamoja na mambo mengine inazingatiwa.
"Tumetembelea mradi wa ujenzi wa hospitali yetu ya Wilaya nimeridhishwa na ujenzi unaoendelea inatekelezwa vizuri sana, pia tumetembelea shule za Sekondari ambazo zimejengwa awamu hii, tumetembelea shule ya Sekondari Lucy Lameck, shule ya Sekondari Msandaka ambapo tumekamilisha ujenzi wa bweni la wavulana,"
Pamoja na mambo mengine ameishukuru serikali kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa shule kongwe zilizopo katika Manispaa hiyo ambazo zilijengwa miaka 50 iliyopita.
"Naleta salamu za upendo za Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupokea mipango yote tuliyopeleka kwa ajili ya Jimbo la Moshi mjini na imetejekezwa,"amesema Mbunge huyo
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa madarasa katika shule ya Sekondari Mawenzi, Afisa Elimu Sekondari Manispaa ya Moshi, Agness Luwhavi amesema serikali imetoa zaidi ya Sh234 milioni kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 9 katika shule ya Sekondari Mawenzi ambayo ujenzi wake umekamilika.
Amesema ujenzi wa madarasa haya ni moja ya nia ya Serikali ya kuhakikisha inaboresha miundo mbinu ya kufundishia na kujifunzia kwa wanafunzi.
"Tunaishukuru serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizi za vyumba 9 vya madarasa kwa manufaa ya kikazi cha Sasa na cha baadaye,"amesema
Naye, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Mwajuma Nasombe ameishukuru serikali kwa kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwemo kwenye miradi ya shule, hospitali pamoja na barabara.
"Tunaishukuru serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea fedha nyingi za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya Manispaa yetu,"amesema Nasombe
MOSHI MANISPAA KILIMANJARO
Sanduku la barua: P.O BOX 318 MOSHI
Simu: +255-027-2752906
simu ya Mkononi: +255-027-274371/4
Barua Pepe: md@moshimc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Manispaa ya Moshi