Halmashauri ya Manispaa ya Moshi imezindua magari mapya matatu ya uzoaji taka ikiwa ni juhudi za kumuunga Mkono Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Joseph Magufuli za kuhakikisha Mji wa Moshi unaendelea kufanya vizuri katika nyanja ya usafi na utunzaji wa mazingira.
Uzinduzi wa magari hayo mapya umefanywa na Mkuu wa Wilaya ya Moshi Kippi Warioba katika viwanja vya ofisi za manispaa Moshi na kuifanya Manispaa kuwa na idadi ya magari nane ya kisasa kwa ajili ya uzoaji wa taka ngumu.
Akizundua magari hayo Kippi Warioba alisema kuwa Manispaa ya Moshi imekuwa ikifanya vizuri kwa muda mrefu kwenye suala la usafi na utunzaji wa Mazingira hivyo ujio wa magari hayo utaifanya iendelee kufanya vizuri zaidi huku washindani wake wakiwa ni Manispaa na Majiji na siyo Halmashauri .
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi Michael Mwandezi, magari hayo matatu ambayo ni compactor mbili(magari ya kushindilia taka) na skip master moja (gari la kubeba maghuba ya taka) yote kwa pamoja yana thamani ya ths. milioni 613, 522,000 ambayo yataamaliza tatizo la uzoaji taka kwa kuzoa taka tani 96 kwa siku.
Alisema kuwa halmashauri ilikuwa na magari matano ambayo yalikuwa na uwezo wa kuchukua kiasi cha tani 156 za taka kwa siku ambapo kwa Manispaa ya Moshi yenye wakazi takribani 206,728 inazalisha taka tani 238 kwa siku.Baada ya kuongeza magari haya ya kisasa yenye uwezo mkubwa wa kubeba na kushindilia taka manispaa ya Moshi itakuwa na uwezo wa kuchukua taka zote zinazozalishwa kwa siku.
Kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Moshi alisema Manispaa Raymond Mbowe alisema Manispaa ya Moshi ipo kwenye mchakato wa ujenzi wa dampo la kisasa pamoja na kujenga kiwanda kitachotengeneza mbolea kwa kutumia takataka ambacho kitatoa fursa ajira kwa wananchi na kugeuza takataka kuwa mali.
Alisema lengo la Manispaa ya Moshi ni kuendelea kuwa kinara wa katika usafi na utunzaji wa Mazingira hapa nchini hivyo watahakikisha wanayatunza magari mapya pamoja na kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya matengenezo ya magari ya uzoaji taka ili kuweza kutekeleza vyema suala la usafi wa mazingira.
“Pamoja na kununua magari haya matatu Manispaa ya Moshi imeanza mchakato wa kununua gari lingine la kisasa kwa ajili ya uzoaji wa taka kwa fedha zilizotengwa kwenye bajeti ya mwaka 2018/2019”Alisema
MOSHI MANISPAA KILIMANJARO
Sanduku la barua: P.O BOX 318 MOSHI
Simu: +255-027-2752906
simu ya Mkononi: +255-027-274371/4
Barua Pepe: md@moshimc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Manispaa ya Moshi