HALMASHAURI ya Manispaa ya Moshi imeanza mikakati ya kuimarisha usafi wa mazingira kwa kuhakikisha utekelezwaji wa sheria ndogo ya usafi na Mazingira ya mwaka 2006 na Marekebisho yake ya mwaka 2019 inafuatwa ili kuendeleza sifa ya Manispaa ya Moshi ya kuwa Manispaa safi ikilinganishwa na Manispaa nyingine hapa nchini.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa Ndg. Rashid Gembe ambapo amesema ili kufikia azma hiyo, uongozi wa Halmashauri utahakikisha sheria hii inatekelezwa vilivyo na ukamataji wa wachafuzi na waharibifu wa mazingira watakamatwa na kutozwa faini ya papo kwa papo isiyopungua kiasi cha Shilingi Elfu Hamsini au kifungo cha miezi sita jela.
“Sheria hii inapiga marufuku utupaji wa taka ovyo, utemaji wa makohozi, utiririshaji wa maji ovyo pamoja na kujisaidia ovyo ambapo kwa yeyote atakayetenda makosa hayo atatozwa faini ya papo kwa hapo isiyopungua Shilingi Elfu Hamsini” Alisema Gembe
Mikakakati mingine iliyowekwa ni pamoja na kuboresha mbao za matangazo ili kuelimisha jamii kuhusu usafi na utunzaji wa Mazingira sehemu mbalimbali za mji, kutoa matangazo kwa vipaza sauti kwenye masoko na kituo kikuuu cha mabasi, kupitisha gari la matangazo na kuendelea kushirikiana na vyombo vya Habari ili kuwakumbusha wakazi wa Manispaa ya Moshi wajibu wao juu ya usafi na utunzaji wa Mazingira.
Aidha alisema mikakati hiyo itahusisha pia ukusanyaji wa taka za aina mbalimbali zinazozalishwa katika mitaa yote ndani ya Manispaa na sehemu ya taka hizo zitatumika kwa ajili ya uzalishaji wa mbolea kwenye Kiwanda cha mbolea cha mboji kilichoko eneo la Mtakuja kinachomilikiwa na kuendeshwa na Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kwa kushirikiana na Mji rafiki wa Tubingen uliopo chini Ujerumani.
“Hadi kufikia mwezi Agosti, mwaka huu, takwimu zinaonesha kuwa mji wa Moshi unazalisha jumla ya tani 236 za taka kila siku yakiwemo mabaki ya mboga mboga na matunda ambayo ni mali ghafi ya Kiwanda cha mboji na uzalishaji huo ni sehemu ya kuufanya mji wetu uwe safi”, alisema.
Gembe alisema nia ya mpango huo kabambe ni kuhakikisha Manispaa ya Moshi inandelea kushika nafasi yake ya kwanza katika Mashindano ya Usafi wa Mazingira yanayofanyika kila mwaka kwa uratibu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii.
“Ushindi wetu wa kila mwaka kwa miaka mingi mfululizo ulikuwa chachu ya miji mingine hapa nchini kuiga mfano wetu katika kuhakikisha mji unakuwa safi ambapo Halmashauri nyingi zimefanya ziara za mafunzo kuja kujifunza jinsi tulivyofanikiwa kufanya mji wetu kuwa safi na kuwa kinara wa usafi hapa nchini”, alisema.
MOSHI MANISPAA KILIMANJARO
Sanduku la barua: P.O BOX 318 MOSHI
Simu: +255-027-2752906
simu ya Mkononi: +255-027-274371/4
Barua Pepe: md@moshimc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Manispaa ya Moshi