Halmashauri ya Manispaa ya Moshi na Jiji la Marburg Ujerumani zimesaini Makubaliano ya Kiungwana kwa ajili ya ushirikiano katika Sekta ya Afya, Michezo na Nyanja mbalimbali zinazohusiana na masuala ya maendeleo ya jamii.
Makubaliano hayo yamesainiwa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi Mhandisi Zuberi Kidumo na Mstahiki Meya wa Jiji la Marburg Dkt. Thomas Spies, katika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa Moshi, mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi Mhandisi Zuberi Kidumo alisema ushirikiano wa Miji hii Miwili vile vile utahusisha ushirikiano katika sekta za Majanga na Zimamoto.
“Marburg ni Jiji ambalo limejikita kwenye masuala ya elimu zaidi hususani ile inayohusiana na afya tib ana kinga hivyo ushirikiano huu utakuwa ni muhimu sana katika kuboresha sekta ya afya katika Manispaa yetu”, alisema.
Aidha alisema Jiji la Marburg pia limebobea katika kupambana na Majanga eneo la uokoaji hasa Zimamoto hivyo uhusiano huu utasaidia kupata vifaa vya Zimamoto Pamoja na Elimu juu ya uokoaji na kupamabana na Majanga kama vile mafuriko na matetemeko ya ardhi.
“Ujumbe wa Mstahiki Meya wa Marburg na ujumbe wake watatembelea kituo chetu cha zimamoto, maeneo ya kutolea huduma za afya yaliyo chini ya Halmashauri ya Manispaa Moshi, ili kujionea shughuli zinazofanyika ili kuweza kupata mwanga wa jinsi ya utekelezaji wa ushirikiano wetu mpya tulioingia rasmi leo tarehe 25/10/2023 ”, alisema.
Mstahiki Meya Kidumo pia alisema ujumbe huo utatembelea miradi ya michezo inayotekelezwa Manispaa ya Moshi ikiwemo ukarabati wa uwanja wa michezo wa Majengo pamoja na vituo vya kukuzia vipaji vya michezo.
“Katia ujumbe huu pia kuna Mtaalamu wa michezo ambaye tayari ameoneysha nia ya kusaidia kukuza vipaji vipya kwa kutoa ufadhili na msaada wa kiufundi katika vituo vya kukuza vipaji Manispaa ya Moshi”, alisema.
Vile vile Mstahiki Meya alisema ndani ya makubaliano hayo tunategemea watumishi wa Jeshi letu la Zimamoto wanatakuwa wanapata mafunzo ili kuboresha hali ya uokoaji na kupambana na majanga mbalimbali yanapotokea.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Jiji la Marburg Dkt. Spies alielezea kufurahishwa kwake na kuanzisha Uhusiano huu mapya kati ya Miji hii Miwili na kuongeza kuwa Uhusiono huu unalenga kuboresha maisha ya wananchi wa pande zote mbili.
“Kwa miaka mingi wananchi wa Marburg wanaamini katika ushirikiano na Halmashauri za Manispaa na Majiji mengine na Moshi ni eneo lao la saba katika kuanzisha ushirikiano wa aina hii”, alisema Dkt. Spies
Alisema wazo la kuunda ushirikiano kati ya Manispaa ya Moshi na Jiji la Marburg ni katika kubadilishana mawazo, kushirikiana katika kutambua na kufuatilia tamaduni za pande zote mbili na pia kila upande kupata fursa ya kujifunza utamaduni ya upande mwingine.
MOSHI MANISPAA KILIMANJARO
Sanduku la barua: P.O BOX 318 MOSHI
Simu: +255-027-2752906
simu ya Mkononi: +255-027-274371/4
Barua Pepe: md@moshimc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Manispaa ya Moshi