MSTAHIKI Meya wa Halmashauri Manispaa ya Moshi Mhandisi Zuberi Kidumo amesema hakuna dhambi wala kosa aina yoyote kumpongeza au kumsifia Rais Dr Samia Suluhu Hassan kwa utendaji kazi wake mzuri na ule wa serikali ya awamu ya sita kwa ujumla.
Msatahiki Kidumo alieleza hayo wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kilichokaa jana kujadili taarifa ya utendaji wa Baraza hilo kwa mwaka wa fedha wa 2022-2023.
“Kupitia taarifa hii tumeona jinsi Halmashauri yetu imepata mafanikio makubwa kutokana na fedha kutoka Serikali kuu pamoja na zile zilizotokana na mapato ya ndani; hivi kuna dhambi gani kumshukuru au hata kumsifu kiongozi wa serikali iliyoleta fedha hizo”, alihoji Mstahiki Meya .
Alisema amelazimika kutoa dukuduku hilo kutokana na kile alichosema ni lawama anazopata kwa watu pale anapotoka kuelezea kazi nzuri zinazofanywa chini ya usimamizi wa Rais Dr Samia.
“Kama wao hawaoni utendaji mzuri wa Rais, sisi ambao ni wasaidizi wake tunaziona hivyo ni vyema tukautaarifu umma kuhusu yaliyofanyika ili wale wasio na uelewa wa jinsi Serikali inavyochangai maendeleo yao na ya nchi kwa ujumla wapate uelewa huo”, alisema.
Akiwasilisha taarifa hiyo, Meya Kidumo alisema kuwa katika sekta ya elimu katika Shule za Msingi na Awali madarasa yameongezeka kutoka 507 mwaka wa fedha 2021/2022 hadi kufikia 530 kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 na Sekondari madarasa yameongezeka kutoka 268 kwa mwaka 2021/2022 na kufikia 317 kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Alisema, “Katika kipindi hicho idadi ya madawati Shule za Msingi imeongezeka kutoka 11,490 na kufikia 11,730, wakati katika Shule za Sekondari idadi hiyo imeongezeka kutoka 11,400 hadi 11,500”.
MOSHI MANISPAA KILIMANJARO
Sanduku la barua: P.O BOX 318 MOSHI
Simu: +255-027-2752906
simu ya Mkononi: +255-027-274371/4
Barua Pepe: md@moshimc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Manispaa ya Moshi