Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, imetoa mafunzo ya sheria ndogondogo na maadili kwa Madiwani, lengo likiwa ni kukumbushana masuala ya maadili na kuimarisha ushirikiano kati ya madiwani na watendaji ili kuboresha ukusanyaji wa mapato ya ndani.
Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna
Mghwira, alisema Mafunzo haya yatakuwa chachu kwa Madiwani na kuboresha ushirikiano kati ya madiwani na watendaji kwa nia ya kuwaletea maendeleo wakazi wa Manispaa ya Moshi.
Alisema lengo la Msingi la mafunzo hayo ni kuwawezesha Madiwani,
kupata uelewa wa sheria ndogondogo za ukusanyaji wa ada na ushuru
mbalimbali kwa ajili ya kuiwezesha Halmashauri, kupata mapato ambayo
yatafanikisha na kurahisisha utekelezaji wa shughuli za utoaji huduma
bora kwa wananchi.
Mghwira alisema Ushirikiano katika utumishi wa Umma unajengwa katika
msingi wa mgawanyo wa majukumu ya kiutumishi, na kuwataka madiwani
kutumia mafunzo hayo kuibua ushirikiano mpya katika
utendaji kazi wakishirikiana na watendaji wa Halmashauri .
"Waheshimiwa Madiwani, ninyi ni watumishi wa umma kwa kuwa mnashika
nafasi ambazo mnawatumikia wananchi,hivyo mafunzo haya ya sheria
ndogondogo za ada na ushuru mbalimbali pamoja na maadili,yawezeshe
kuwepo kwa ushirikiano wa pamoja kati yenu na watendaji,katika suala
zima la ukusanyaji wa mapato ndani ya Halmashauri"alisema Mghwira.
Mkuu wa Mkoa alitumia pia nafasi hiyo kuwataka madiwani kutumia
mafunzo hayo, kufanikisha shughuli za ukusanyaji wa
mapato,utayarishaji wa taarifa fasaha,sahihi na za kuaminika, ambazo
zitatumika kama rejea katika kuamua mwelekeo wa Halmashauri katika
suala zima la Mapato.
Akizungumza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi,
Bwana Michael Mwandezi, alisema watazingatia mada zote
zitakazofundishwa kwani zitasaidia kuiwezesha Halmashauri yake kukusanya
mapato yaliyokusudiwa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya madiwani walioshiriki mafunzo hayo,walisema mafunzo watakayoyapata yatakuwa chachu ya kuwawezesha kusimamia na
kutekeleza sheria ndogondogo za ukusanyaji wa Mapato ya Halmashauri, pamoja na kuzingatia maadili ya utumishi wa Umma.
MOSHI MANISPAA KILIMANJARO
Sanduku la barua: P.O BOX 318 MOSHI
Simu: +255-027-2752906
simu ya Mkononi: +255-027-274371/4
Barua Pepe: md@moshimc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Manispaa ya Moshi