Mafanikio ya Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, kushawishi wananchi wake kuchangia ada ya taka kwa ajili ya ukusanyaji na uzoaji taka katika ngazi ya kata ‘umeziduwaza’ halmashauri za Jiji la Mwanza, Manispaa ya Ilemela na Manispaa ya Morogoro.
Mkuu wa Idara ya Usafi na Mazingira wa Jiji la Mwanza, Viane Kombe alisema mafanikio hayo ya Moshi, ndiyo yaliyowasukuma maafisa afya na watendaji wa kata katika halmashauri hizo tatu kutembelea Manispaa ya Moshi kujifunza masuala ya usafi na utunzaji wa Mazingira pamoja na jinsi ya kugeuza taka kuwa mali.
“Kuja kwetu Moshi ni kutaka kujifunza wenzetu wanafanyaje usafi, siri ya mafanikio yao na gharama halisi za kuendesha zoezi la ukusanyaji taka mitaani, wao wametwaa mara nyingi tuzo za mashindano ya taifa ya afya na usafi wa mazingira inayohusisha halmashauri za majiji, manispaa, miji na wilaya 73 nchini,”alisema
Manispaa ya Moshi iliendelea kuongoza halmashauri majiji na manispaa baada ya kuwa mshindi wa kwanza kitaifa mwaka jana kwa kupata asilimia 78.5, ikifuatiwa na Jiji la Arusha iliyopata asilimia 78.1 na Manispaa ya Iringa asilimia 67.2
Akitoa siri ya mafanikio hayo, Afisa Mtendaji wa Kata ya Mawenzi, Erasmo Silayo alisema eneo lake ambalo lina kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani na ambalo ndio kitovu cha mji huo limejiwekea utaratibu mzuri wa ukusanyaji fedha za usafi, ambapo kwa mwaka mmoja hukusanya kiasi cha Sh. milioni 45 kama ada.
Fedha hizo hutumika kulipa vibarua 17 wanaofanya kazi ya kufagia mitaani na wale wanaotembea na magari ya taka, kununua mafuta ya gari linalohudumia kata hiyo mara tatu kwa wiki.Wananchi humasishwa kuhifadhi takataka katika vyombo vya kuhifadhia taka ngumu na huzitoa taka hizo wakati ambapo gari linapopita.
“Wananchi wetu wamejengewa utaratibu wa kuchangia ada ya uzoaji taka, tumekuwa tukitoa demand notes (hati ya madai) kila mwanzo wa mwaka wa fedha, kwa biashara zote na ngazi ya kaya, tuna viwango tofauti, kwa mfano kwa wafanyabiashara tunaanzia 780,000 mpaka 36,000 ambayo ni kiwango kidogo kabisa. Katika ngazi ya kaya tunachukua shilingi 12,000 kwa mwaka kwa maana ya kwamba kila mwezi kaya inachangia shilingi 1, 000”alifafanua Silayo
Aidha, Kaimu Mkuu wa Idara ya Usafi na Mazingira wa Manispaa ya Moshi, Bernadeta Mtei alisisitiza pamoja na mafanikio hayo, Manispaa hiyo kwa siku moja inazalisha kiasi cha tani 256 za taka na kwamba kwa wale wachache ambao ni wakaidi kuchangia ada ya taka hufuatiliwa na uongozi wa kata na kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria ndogo ya Halmashauri ya Manispaa ya Moshi ya Mwaka 2006 pamoja na Marekebisho yake.
MOSHI MANISPAA KILIMANJARO
Sanduku la barua: P.O BOX 318 MOSHI
Simu: +255-027-2752906
simu ya Mkononi: +255-027-274371/4
Barua Pepe: md@moshimc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Manispaa ya Moshi