SERIKALI ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha sekta ya afya kupitia fedha za tozo ambapo safari hii jumla ya shilingi milioni 250 zilizotolewa kwa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi zinatarajiwa kutumika katika kuboresha kituo cha afya cha Shirimatunda kilichopo Kata ya Shirimatunda.
Mkurugenzi wa Manispaa Ndg. Rashid Gembe amesema fedha hizi zitatumika katika upanuzi wa kituo hicho kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya Mama na Mtoto, jengo la upasuaji, njia ya kupitia wakati wa kutoa na kupata huduma (walkway) na jengo la kufulia.
“Moboresho haya yatasaidie kutoa huduma kwa karibu zaidi kwa wagonjwa ambao walikuwa wakisafiri mwendo mrefu kutoka kata ya Shirimatunda na Kata za jirani kwenda hospitali ya rufaa ya Mkoa au ile ya rufaa ya Kanda ya KCMC kufuata huduma ambazo zitapatikana baada ya maboresho ya kituo hiki”, alisema.
Gembe aliendelea kusema kuwa mbali na wakazi wa kata ya Shirimatunda, Soweto na Karanga kunufaika na maboresho hayo pia wananchi walioko maeneo ya vijiji vya Shirimgungani na Mijengweni wilaya ya Hai watanufaika na maboresho hayo.
Kwa mujibu wa Gembe hiyo ni awamu ya pili ya fedha kutolewa na Serikali kwa ajili ya maboresho ya kituo hicho cha Shirimatunda kufuatia jumla ya shilingi milioni 250 zilizotolewa awali ambazo alisema zilifanikisha ujenzi wa jengo la kutoa huduma kwa wagonjwa wa nje (OPD) na maabara katika kituo hicho jambo ambalo alisema limewaongezea ari ya kufanya kazi wahudumu walioko kituoni hapo.
“Mbali na watumishi kuridhika, maboresho haya pia yamewahamasisha wananchi na kusababisha idadi ya watu wanaopata huduma katika kituo hicho kuongeza kutoka wastani wa watu 20 na 25 kwa siku na kufikia 30 na 35 kwa siku”, alisema.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi Mhandisi Zuberi Kidumo ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha hizo za Tozo ambapo amesema kuboreshwa kwa huduma katika kituo hichi ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025 lengo lake ni kutoa huduma bora na kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.
“Nichukue fursa hii kwa niaba ya wananchi wa Manispaa ya Moshi kuipogeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ilivyokuwa mstari wa mbele katika kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi na jinsi ilivyokuwa mstari wa mbele kuboresha huduma za afya na kusogeza huduma hizo kwa wananchi.”, alisema.
MOSHI MANISPAA KILIMANJARO
Sanduku la barua: P.O BOX 318 MOSHI
Simu: +255-027-2752906
simu ya Mkononi: +255-027-274371/4
Barua Pepe: md@moshimc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Manispaa ya Moshi