Watumishi Halmashauri ya Manispaa ya Moshi wametakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya haki na kuepuka dhuluma kwa wale wanaowaongoza na kuwasimamia.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Manispaa Bi Mwajuma Nasombe wakati akifungua kikao kazi cha watumishi viongozi katika ngazi ya Kata na Mitaa wa Manispaa, kilichofanyika katika ukumbi wa shule ya sekondari Moshi.
Nasombe amesema watumishi wote waliopewa dhamana ya uongozi, wanapaswa kusimama kwenye haki na kutanguliza mbele maslahi ya Taifa, ili kuwezesha dhamira ya serikali ya kuwaletea wananchi maendeleo kufikiwa kikamilifu.
"Tusiache kumtanguliza Mungu kwenye kila tunachofanya, niwakumbushe watumishi wenzangu, hakuna kitu kibaya kama dhuluma, dhuluma ni mbaya, wakati mwingine unaweza kuona unafanya mambo yako hufanikiwi, kumbe kuna nafsi zinalia kwa ajili yako, unashangaa kila unachofanya hakiendi mbele, kumbe unawadhulumu watu wengi na machozi ya watu wasiokuwa na hatia, lazima uyalipie, usipolipa wewe watalipa kizazi chako"Alisema Nasombe
Aidha aliwataka watumishi wa umma kujua majukumu yao na wajibu wao kwa jamiii na ni lazima wajue wanawajibika katika maeneo gani na wakati gani wanatakiwa kufanya nini na pia wanatakiwa kusema nini.
"Watumishi wenzangu, tunakwenda kwenye maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu, vibweka hapa katikati vitakuwa vingi sana, usishawishike kuzungumza kitu ambacho hukifahamu na sitarajii kukuona unazungumza beyond (zaidi) ya mipaka yako, lakini sitarajii zaidi ukizungumza vitu ambavyo vitakwenda kupasua taifa hili, mimi kama kiongozi wenu ninatamani tutembee pamoja".
Katika hatua nyingine, Nasombe aliwataka viongozi hao kusimamia fedha za miradi kwa uadilifu na kuhakikisha kila fedha inayoingia kwa ajili ya utekekezaji wa miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao, wanashirikisha watalaamu wa Manunuzi ili kuepuka matumizi mabaya ya fedha.
MOSHI MANISPAA KILIMANJARO
Sanduku la barua: P.O BOX 318 MOSHI
Simu: +255-027-2752906
simu ya Mkononi: +255-027-274371/4
Barua Pepe: md@moshimc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Manispaa ya Moshi