BARAZA la madiwani la Halmashauri ya manispaa ya Moshi, limeazimia kuandika barua kwa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kushawishi kukifunga kiwanda cha ngozi cha Moshi kwa madai ya kukiuka sheria za mazingira na kuathiri afya za wananchi.
Kiwanda hicho kilichopo katika kata ya Njoro, kimekuwa kikilalamikiwa kwa muda mrefu na wananchi kutokana na kutoa harufu mbaya inayosambaa katika makazi yao hali ambayo imekuwa ikiathiri afya zao .
Akitoa azimio hilo kwa niaba ya wajumbe wa baraza , Naibu mstahiki meya Peter Minja, alisema kiwanda hicho kimegeuka kero kwa wananchi kutokana na kukiuka sheria za mazingira kwa muda mrefu hali ambayo imekuwa ikihatarisha afya za wakazi wa eneo hilo.
Alisema licha ya halmashauri kufanya jitihada za kuhakikisha mwekezaji wa kiwanda hicho anafuata taratibu, na sheria za mazingira ikiwemo kuthibiti harufu hiyo ambayo imekuwa kero kwa wananchi, amekuwa kitoa ahadi ambazo hazitekelezi .
“Mkurugenzi tunakuagiza uandike barua NEMC ueleze namna harufu hii inavyo waathiri wananchi afya zao.”alisema
Aliendelea kusema kuwa “Barua hii iandikwe haraka iweezekanavyo na isiishie hapo tu… menejimenti tunaomba muende pale kiwandani mfanye ukaguzi kwani muwakilishi wa kiwanda katueleza kuwa kunamashine wamefunga tayari za kutibu maji taka na kuzuia hiyo harufu mjiridhishe kama kweli zoezi hilo limefanyika”alisema.
Akizungumza kabla ya kupitishwa kwa azimio hilo Diwani wa kata ya Bomambuzi Juma Rahibu, alisema kiwanda hicho kwa miaka mingi kimegeuka kero kwa wananchi wanaoishi katika kata hiyo na kata nyingine za pembezoni jambo ambalo halipaswi kufumbiwa macho na mamlaka zinazo husika.
Naye Diwani wa kata ya Rau ,Peter Kimaro alisema kiwanda hicho kimekuwa kikitoa matumaini kwa halmshauri hiyo kwamba wanauwezo wa kudhibiti harufu hiyo tangu mwaka 2013 na kwamba sasa ni miaka mitano imepita na suala hilo bado halijatafutiwa ufumbuzi hivyo ni vema hatua za kisheria zifuatwe ili kunusuru afya za wananchi.
“Kiwanda hichi kilishapigwa faini ya shilingi milioni 32 na NEMC yenyewe kutokana na kukiuka sheria za mazingira lakini pamoja na faini hiyo bado hawajafanya marekebisho yoyote hivyo tuwajulishe ili waone ni taratibu gani za kisheria zinapaswa kufuatwa kwa sasa”alisema Priscus Tarimo Diwani wa Kata Kilimanjaro
Danford Kamenya, kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, alisema watafika kiwandani hapo kufanya ukaguzi ili kuona kama mashine za kudhibiti harufu zimefungwa, kama ilivyokuwa makubaliano ya awali.
“Kiwanda hiki tulikiagiza kifunge mashine za kudhibiti harufu, na zoezi hilo lilitakiwa kukamilika April 2017, lakini walidai kazi hiyo ni kubwa itahitaji muda, na wamekamilisha Disemba 2017, sasa tutakwenda kuwakagua kama wametekeleza hilo na tukikuta hawajafanya, tutaandika barua NEMC ili wao waone ni hatua zipi za kisheria watachukua”alisema Kamenya.
MOSHI MANISPAA KILIMANJARO
Sanduku la barua: P.O BOX 318 MOSHI
Simu: +255-027-2752906
simu ya Mkononi: +255-027-274371/4
Barua Pepe: md@moshimc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Manispaa ya Moshi