Baraza la Madiwani la Manispaa ya Moshi, limepitisha bajeti ya mwaka wa fedha wa 2018/2019 ambayo ni zaidi ya Sh. Bilioni 48.482.
Meya wa Manispaa hiyo, Raymond Mboya alitangaza bajeti hiyo , wakati akifunga kikao cha Baraza la Madiwani kilichoketi kujadili na kuidhinisha mapendekezo hayo ya bajeti.
“Bajeti hii ya Shilingi bilioni 48, 482, 284, 521 tuliyoipitisha leo, inajumuisha miradi ya maendeleo, mishahara na matumizi menginineyo ya Manispaa yetu, lakini mapato ya ndani ni sh. bilioni 6, 259, 680,600 na hii ni pamoja na ongezeko la shilingi milioni 570,”alisema Mboya
Alisema mbali ya baadhi ya vyanzo vya mapato kufutwa na serikali kuu na kupelekea kushuka kwa mapato ya Manispaa hiyo, bado halmashauri ya Manispaa ya Moshi imeweza kupandisha mapato yake kutoka kwenye vyanzo vingine na kuwa kiasi cha sh. bilioni 6.2.
Kutokana na mafanikio hayo, Meya huyo alimwomba Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Michael Mwandezi kuhakikisha bajeti hiyo inafanyiwa kazi.
Akisisitizia kwamba hatua hiyo ni muhimu, Mboya alisema: “Tunaomba juhudi zifanyike katika makusanyo kwa sababu hatujui kesho, kesho kutwa ni mapato gani mengine ambayo yatakusanywa na serikali kuu. Sasa twende kwenye utekelezaji wa kuhakikisha tunayapata haya mapato, naomba nitangaze rasmi hii ya sh. Billion 48,482,284,521 ndio bajeti ya Manispaa ya Moshi kwa mwaka mpya wa fedha 2018/2019.”
Aidha, Meya alisema Manispaa imejipanga kuhakikisha inasimamia miradi hiyo ili ilete mabadiliko ya kiuchumi kwa wananchi na wakazi wa Manispaa ya Moshi .
MOSHI MANISPAA KILIMANJARO
Sanduku la barua: P.O BOX 318 MOSHI
Simu: +255-027-2752906
simu ya Mkononi: +255-027-274371/4
Barua Pepe: md@moshimc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Manispaa ya Moshi