Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kwa kauli moja limepitisha mpango na bajeti ya mwaka wa fedha wa 2025/2026 kwa jumla ya Tshs 53,277,410,316.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi Mhandisi Zuberi Kidumo, alitangaza bajeti hiyo , wakati akifunga kikao cha Baraza la Madiwani kilichoketi kujadili na kuidhinisha mapendekezo ya bajeti na kueleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2025/2026 mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa Shs 9,970,000,000, Matumizi ya kawaida ruzuku ya uendeshaji (OC) ni Shs 1,297,519,000, Miradi ya Maendeleo ni Shs 9,8177,880,316 na kwa upande wa Mishahara inatarajiwa kuwa Shs 32,192,020,000 hivyo kufanya jumla ya Bajeti ya Manispaa ya Moshi kuwa Shs 53,277,410,316.
Awali kabla ya kuwasilisha Bajeti hiyo Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi Bi Mwajuma Nasombe alieleza kuwa Bajeti hii ya mwaka wa fedha 2025/2026 ni Bajeti ya Kimkakati na imezingatia katika Ujenzi wa miradi mikubwa Mitatu kwa ajili ya kuongeza Mapato na kukuza Uchumi wa Manispaa ya Moshi.
“Muheshimiwa Mstahiki Meya napenda kulijulisha Baraza lako kuwa Bajeti ya Mwaka huu tumezingatia miradi mikubwa ya uwekezaji kama vile Ujenzi wa vibanda vya maduka, ukumbi wa mikutano na Ujenzi wa uwanja wa michezo wa Majengo ambavyo vyote hivyo vitatuongezea mapato ya ndani” Alisema Nasombe
Akiwasilisha bajeti hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Mkuu wa Divisheni ya Mipango na Ufuatilia Bi Monica Sana alisema kuwa uundaji wa bajeti ya Manispaa ya Moshi kwa mwaka wa fedha 2025/2026 umezingatia vipaumbele ya Manispaa ambavyo ni kukamilisha miradi viporo,kuboresha ukusanyaji wa mapato kwa kubuni vyanzo vipya na kujenga miradi ya kimkakati ya kuongeza mapato ya ndani.
MOSHI MANISPAA KILIMANJARO
Sanduku la barua: P.O BOX 318 MOSHI
Simu: +255-027-2752906
simu ya Mkononi: +255-027-274371/4
Barua Pepe: md@moshimc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Manispaa ya Moshi